KUKAMATWA KWA MANJI KWAANZA KUIUMIZA KLABU YA YANGA,SASA HALI YAWA MBAYA KIFEDHA,SOMA HAPO KUJUA
YANGA imekiri kuwa na wakati mgumu kiuchumi, lakini
imeapa kupambana kutetea taji lake la Ligi Kuu bara na kufanya vizuri kwenye
michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu wapo nafasi ya
pili kwenye msimamo wakiwa na pointi 49 nyuma ya Simba yenye pointi 54
kileleni.
Yanga
ina faida ya mchezo mmoja kibindoni.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa
Yanga, Charles Mkwasa alisema wana hali ngumu kiuchumi kutokana na Mwenyekiti
na mfadhili Yusuf Manji kupata matatizo, lakini atashirikiana na viongozi
wenzake kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Manji anatuhumiwa kutumia dawa za kulevya na kuajiri
wafanyakazi wa kigeni bila kufuata taratibu, suala linalodaiwa kukwamisha
masuala yake mengi yakiwemo kuigharamia Yanga kama ilivyo siku za nyuma.
“Hatupo vizuri kifedha ni kweli hiyo ni kutokana na
matatizo ya mfadhili wetu hivyo uongozi ndio tunasimamia mambo yote kwa sasa
kuhakikisha hatukwami mahali, ikiwemo ushiriki wetu wa ligi pamoja na michuano
ya kimataifa,” alisema.
Yanga inatarajiwa kucheza na Zanaco ya Zambia katika
mechi ya Ligi ya Mabingwa katikati ya mwezi ujao. Mkwasa aliyewahi kucheza na
kufundisha timu hiyo pia aliajiriwa kwenye nafasi hiyo katikati ya mwezi huu
akichukua mikoba ya Dk Jonas Tiboroha aliyesitishiwa mkataba wake.
Yanga kesho inatarajiwa kushuka kwenye uwanja wa
Taifa kuikaribisha Ruvu Shooting katika mechi yake ya Ligi Kuu ambapo inahitaji
ushindi ili kurudisha imani ya mashabiki wake walioonekana kufadhaika baada ya
kupoteza mechi ya mtani wake mwishoni mwa wiki iliyopita. Akizungumzia mechi
hiyo Mkwasa alisema kila kitu kiko sawa na wanaingia uwanjani kusaka ushindi
kama wanavyofanya kwenye mechi zote.
“Timu imeshasahau yaliyopita na imeshajipanga kwa
mchezo wetu ujao ambao tunatarajia tutashinda ili tuendelee vizuri na kampeni
za kutetea ubingwa,” alisema Mkwasa.
Aidha katika hatua nyingine, Shirikisho la soka
Tanzania (TFF) limerejesha mechi za Ligi Kuu kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro
na Jumapili hii Mtibwa Sugar itaikaribisha Yanga. Awali TFF ilifungia uwanja huo
kutumika kwenye mechi za ligi baada ya kuonekana kuchakaa sehemu ya kuchezea
ikiwa haina nyasi.