Zinazobamba

JUKWAA LA KATIBA: HATUKUBALIANI NA UTAJAJI MAJINA USIO NA TIJA,..


  

Jukwaa la katiba Tanzania (JUKATA) limeibuka na kupinga tabia ya kutaja majina ya watu wanaodaiwa kuhusika na biashara ya madawa ya kulevya pasipo kufuata taratibu za Nchi, wakisema kufanya hivyo kunaweza kuleta athari kubwa kwa watanzania ikiwamo kulipa fidia nyingi kama ikibainika kuwa waliotajwa hawahusiki na biashara hiyo.
 
Akizungumza na Waandishi wa habari, ofisini kwake  Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Bw. Deus Kibamba amesem Jukwaa hilo linaamini katika utawala wa sheria, na kushauri kuwa ni busara kwa vinara wa vita hii kufanya uchunguzi kabla ya kuwataja hadharani na kuchafua maisha ya watu.
 
"Utajaji wa majina una athari mbili moja ni kulipa fidia kama ikibainika waliotajwa hawahusiki, lakini la pili ni muendelezo wa chuki kati ya kizazi na kizazi kutokana na majina hayo. ni heri zoezi hilo likafanywa na watu wenye weledi ambao wamesomea taaluma ya uchunguzi."

Aidha akizungumzia Juu ya kukwama kwa mchakato wa katiba mpya nchini na Jinsi ya kuuanzisha Upya Deus amesema JUKATA wamejipanga kuhakikisha kuwa mchakato huo unahishwa ili taifa lipate katiba mpya.



Katika hatua nyingine JUKATA pamoja na kulaani watu wanaotumia lugha za matusi kuwakosoa viongozi wakuu wa nchi lakini hatua ya kuwakamata na kuwaweka ndani watu kwa makosa ya kukosoa kwa lugha nzuri bila matusi ni kinyume cha katiba ya Tanzania huku wakisisitiza kuwa hakuna kiongozi bora duniani asiyekubali kusikia mawazo ya kukosolewa kutoka kwa  wananchi wake.

Kibamba amesema kuwa uvumilivu wa kisiasa unahitajika sana katika nchi kipindi hichi  ambacho nchi inaongozwa na serikali mpya kwa kuwa kumekuwa na matukio ambayo yanatisha ikiwemo watu kupotea bila kujulikana walipo,na wengine kukutwa wakiwa wamefariki katika viroba na serikali kushindwa kutoa maelezo yaliyokamilika kuhusu matukio hayo.
 
Aidha katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa JUKATA amesema kuwa kulingana na matukio mbalimbali yanayoendelea kutokea nchini sasa ni wazi kuwa nchi inahitaji katiba mpya sasa na sio siku nyingine hivyo wao kama JUKATA wameanza Rasmi mchakato wa kufufua harakati za kupata katiba mpya nchini.

Moja kati ya mambo ambayo ameyataja kuwa wameanza nayo katika kufufua mchakato huo ni pamoja na kufanya mkutano mkuu wa katiba ambao utafanyika kuanzia Tarehe 2 hadi 3 mwezi wa Tatu ambao utawashirikisha wadau mbalimbali wa katika nchini, pamoja na uzinduzi wa Filamu mpya ya Dakika 20 itakayokuwa inaonyesha mchakato mzima wa katiba mpya.
 
Katika hatua nyingine JUKATA wametuma wito wa kufanya mazungumzo na Rais Wa Jamhuri Ya muungano wa Tanzania Mh Dr John Pombe Magufuli kwa ajili ya kujadili naye maswala mbalimbali yanayohusu Katiba mpya nchini pamoja na kumshauri Mambo kadhaa ya kupata katiba Mpya.