Zinazobamba

WANAOKIHUJUMU CHAMA CHA CUF HAWA HAPA,MAALIM SEIF AWATAJA,SOMA HAPO KUJUA



 
Katibu  Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ameibuka na kutaja utatu unaojumuisha mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Jeshi la Polisi akieleza ndio unaoshirikiana kukihujumu chama hicho, huku akibainisha mambo tisa anayoeleza kuwa ‘ushahidi wa ushirikiano’ na hujuma hizo.

Akizungumza katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuibuka kwa mgogoro ndani ya chama hicho baada ya Jaji Mutungi kumtambua profesa Lipumba kuwa  mwenyekiti wa CUF, Maalim Seif alitumia dakika 95 kueleza hujuma hizo na kudai zinalenga kukifanya chama hicho kutodai haki ya kunyang’anywa ushindi wa Uchaguzi Mkuu Zanzibar.

Akiwa sambamba na viongozi mbalimbali wa chama hicho, alisema hana ugomvi na Profesa Lipumba na yupo tayari kukaa naye meza moja kueleza uongo wa mtaalamu huyo wa uchumi, ikiwa ni pamoja na ukweli anaouficha kuhusu kujiuzulu kwake uenyekiti wa CUF Agosti mwaka jana na uamuzi wake wa kutaka kurejea katika chama hicho.


Mbali na kukiri CUF kupitia katika wakati mgumu kwa sasa, Maalim Seif alisema hujuma hizo zilizotokana na ‘wakubwa’ kuchukizwa na kitendo cha chama hicho kuwasilisha vielelezo Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC) vinavyowatuhumu viongozi wa Serikali kutumia mamlaka yao vibaya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana,  zimesababisha chama hicho kutopata ruzuku ya Sh milioni 117 kila mwezi, tangu Agosti mwaka huu.

“Mtiririko wa matukio haya (tisa) yanaonesha wazi  hujuma hizi…, ni  mambo yanayoratibiwa kwa suhirikiano wa  makusudi  kati ya msajili, polisi na Lipumba, “ alisema Maalim Seif.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kuvamiwa kwa Mkutano Mkuu wa CUF iliofanyika Agosti 21, utekaji wa wanachama na viongozi wa chama hicho, kuvamiwa kwa ofisi kuu iliyopo Buguruni, kuvunjwa kwa ofisi za wilaya ya Bagamoyo na Mkuranga, wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho kuzuiwa kufanya kikao cha ndani.

Mengine ni kuzuiwa kufanyika kwa mkutano mkuu maalumu wilaya ya Tanga, utekaji wa mlinzi wa chama hicho uliofanyika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuzuiwa kwa kikao cha ndani mkoani Mtwara pamoja na walinzi wa Profesa Lipumba kutaka kuzuia viongozi wa CUF kuingia chumba cha mahakama kuu hiyo.

Agosti 8 mwaka jana Profesa Lipumba alitangaza kuachana na uongozi wa chama hicho, baada ya CUF kukubaliana na Ukawa kumsimamisha Edward Lowassa kuwania urais.

Hata hivyo, Juni mwaka huu Profesa huyo aliomba kwa barua kurejea kwenye wadhifa wake, ambao kwa sasa unashikiliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro aliyechaguliwa katika mkutano wa  Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho.

Uamuzi wake huo ulizua  sintofahamu ndani ya CUF  huku mkutano mkuu wa dharura wa chama hicho uliofanyika Agosti 21 mwaka huu kumchagua mwenyekiti mpya ukivunjika baada ya kundi la wafuasi wa chama hicho kuvamia na kufanikiwa kuzima mchakato wa kupiga kura kumchagua mwenyekiti mpya, wakishinikiza Profesa Lipumba aruhusiwe kurejea katika wadhifa huo.

Baada ya sakata hilo Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho lilimvua uanachama Profesa Lipumba na kuwasimamisha uanachama makada kadhaa wa CUF, jambo ambalo liliingiliwa kati na Msajili wa Vyama vya Siasa aliyetoa waraka wa kumtambua Lipumba kuwa mwenyekiti.

Kitendo cha Lipumba kutambuliwa na kurejea katika chama hicho kilisababisha Baraza la Wadhamini la CUF kufungua kesi Mahakama Kuu na kumshtaki profesa huyo  Jaji Mutungi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju.

Katika ufafanuzi wake, Maalim Seif alisema Lipumba alivamia Mkutano Mkuu wa chama hicho akiongozwa na polisi na kusababisha vurugu kubwa sambamba na uharibifu wa mali lakini polisi haikuchukua hatua yoyote.

“Kumekuwa na matukio kadha aya utekaji wa viongozi na wanachama wa CUF…, mkurugenzi wetu wa fedha Joram Bashange alitekwa akiwa anatoka nyumbani kwake na walinzi wa Lipumba, licha ya kukamatwa na kufikishwa polisi waliachiwa na gari walilotumia nalo halipo kituo cha polisi buguruni,” alisema.

Alisema Septemba 24 mwaka huu, Lipumba na wafuasi wake walivamia ofisi kuu ya CUF iliyopo Buguruni na kufanya uharibifu huku akipewa ulinzi mkali wa polisi.

“Polisi kazi yao ni ulinzi wa raia na mali zao pamoja na kupambana na wahalifu lakini hivi sasa wao ndio wanatetea wahalifu. Tunamuomba Mwigulu (Nchemba-Waziri wa Mambo ya Ndani) kuingilia kati na kutizama watendaji walio chini ya wizara yake,” alisema Maalim Seif.

Alisema tukio la nne ambalo polisi imeshindwa kukamata wahusika licha ya kuwajua ni uvamizi uliofanywa na wafuasi wa Lipumba wa kuvunja ofisi za chama hicho wilayani Bagamoyo na Mkuranga.

“Wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu la uongozi la chama walizuiwa kufanya kikao cha ndani Newala na kukamatwa walipokuwa Nachingwea,” alisema na kubainisha kuwa wakati viongozi hao wakikamatwa, Lipumba anafanya vikao kama hivyo bila kukamatwa.

“Polisi walizuia kufanyika kwa mkutano mkuu maalum wa wilaya ya Tanga kwa madai kuna pande mbili zinavutana. Pia Novemba 10 mwaka huu mlinzi wa chama, Mohamed Said alitekwa akiwa mahakama kuu na kupigwa sana na kunyang’anywa fedha na kupelekwa kuhojiwa na Lipumba. Tukio hilo lilitokea mbele ya polisi,” alisema.

Alisema jeshi hilo pia lilizuia kufanyika kwa kikao cha ndani mkoani Mtwara pamoja na walinzi wa Lipumba kutaka kuzuia viongozi wa CUF kuingia ndani ya chumba cha mahakama kufuatilia shauri lao, huku akimtaja mmoja wa walinzi hao kuwa ni Hassan Kingwele.

Akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Lipumba, Maalim alisema msomi huyo anatumiwa na dola  na kubainisha kuwa anaficha ukweli juu ya uamuzi wake wa kujiondoa CUF.

“Lipumba bado hajasema sababu za kweli juu ya kujiuzulu kwake, yeye ndio alikuwa mwanzilishi wa Ukawa katika Bunge Maalum la Katiba na ndio aliyemtafuta Lowassa na kumshawishi awanie urais kupitia Ukawa,” alisema.

“Lowassa ilikuwa ajiunge na NCCR kwa sababu ni chama kidogo ili CUF na Chadema tumuunge mkono kwa mantiki hiyo iweje Lipumba aseme mimi sikumshirikisha ujio wa Lowassa ndani ya Ukawa?”

Alisema yeye hana ugomvi na Lipumba bali mtaalam huyo wa uchumi ana ugomvi na CUF, huku akidai kuwa hivi sasa anatumia udini, ukabila na uzanzibari kukigawa chama hicho.

“Hizi ni jitihada za dola kunifanya nisidai haki kwa yaliyotokea Zanzibar…, hilo halitawezekana nitaidai tu mpaka mwisho,” alisema.