Zinazobamba

MBUNGE KUBENEA AMLIPUA WAZIRI NAPE,SOMA HAPO KUJUA

Saed Kubenea, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited
SAED Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers, wachapishaji wa magazeti ya MwanaHALISI, MSETO na MAWIO amesema Muswada wa Upatikanaji wa Habari utakaowasilishwa Bungeni wiki ijayo ‘utaua’ vyombo vya habari, anaandika Charles William.
Muswada huo unaojulikana kama Sheria ya Huduma za Habari – The Media Services ACT (2016), unatarajia kusomwa kwa mara ya pili na iwapo utapitishwa, utakuwa mbadala wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na wanahabari kwa miongo mitano sasa.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara eneo la Manzese, Bakhresa jijini Dar es Salaam, Kubenea amesema muswada huo si tu utaviathiri vyombo vya habari bali pia utazima sauti za wananchi.
“Muswada huu ni kitanzi cha uhuru wa kupokea na kusambaza habari unaotajwa katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania, sisi kama wabunge wa upinzani tutaupinga kwa nguvu zote.
Muswada unasema Ofisa wa Polisi yaani IGP anaweza kuamuru mtambo uliochapisha gazeti lililofanya kosa au kurusha matangazo yatakayoonekana maudhui yake yamekiuka sheria uchukuliwa na kutaifishwa hata kama mtambo huo si mali ya mkosaji,” amesema.
Kubenea pia amepinga suala la kuanzishwa kwa Bodi Huru ya wandishi wa habari ambayo wajumbe wake watateuliwa na waziri wa Habari, Vijana, Sanaa na Michezo na kusema bodi hiyo haiwezi kuwa huru na badala yake itakuwa ikifanya kazi ya kuminya uhuru wa habari.
“Kwanini Bodi ya Wahandisi haiundwi na waziri wa miundombinu? Kwanini Bodi ya Madaktari au Wafamasia haiundwi na waziri wa afya? kwanini Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), hakiundwi na waziri wa Katiba na Sheria lakini Bodi inayoitwa Huru ya waandishi wa habari itaundwa na Nape?” amesema.
Ameongeza kuwa bodi itakayoundwa na Nape kwa mujibu wa muswada huo ndiyo itakayokuwa ikitoa leseni kwa waandishi wa habari na kwamba itakuwa na mamlaka ya kuamua nani apewe leseni hiyo, nani asipewe na nani anyang’anywe jambo litakaloweza kuleta athari kubwa kuliko hata sheria za sasa.
“Watakaoathirika si wanahabari tu kwasababu muswada unasema mtu atakayetengeneza au kueneza taarifa za uongo au uzushi unaoweza kuwatia hofu wananchi akipatikana na hatia atatozwa faini isiyopungua Sh. 10 milioni mpaka Sh. 20 milioni au kifungo cha miaka minne mpaka sita,” amesisitiza.