MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA AENDELEA NA KITUKO CHAKE,SASA AMGEUKA LIPUMBA WAKE,SOMA HAPO KUJUA
Wakati wanasiasa na wasomi wakimnyooshea
kidole Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi (pichani) kwa uamuzi
wake wa kumtambua aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba,
mwenyewe ameibuka na kusema kuwa hatua yake hiyo haikulenga kumrudishia msomi
huyo nafasi yake ya uenyekiti.
Jaji Mutungi jana alisema kuwa alichofanya ni
kukishauri chama hicho kuhusu mgogoro uliokuwa ukikisonga na Lipumba
aliamua kutumia ushauri huo kurudi mwenyewe kwenye nafasi yake hiyo kinyemela.
Kauli hiyo ya Jaji Mutungi imekuja siku mbili tangu
alipotoa waraka unaoelezwa kumtambua Profesa Lipumba kama kiongozi halali wa
CUF licha ya kuandika barua ya kujiuzulu Agosti 6, mwaka jana akipinga vyama
vinavyounda Ukawa kumpa fursa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kugombea
urais.
“Isome barua yangu…, mimi nimeamua watu
waijadili umenielewa? Ni vizuri wanavyoijadili, ila nilitarajia waijadili kwa
tija sio kwa hasira,”alisema Jaji Mutungi.
Alipoulizwa kuhusu polisi kumsaidia Profesa Lipumba
kuingia katika makao makuu ya CUF kwa mtutu alisema: “Hizo ni taratibu
ambazo (polisi) wanatumia kwa kuzingatia sheria nyingine za nchi.”
Juni mwaka huu, Profesa Lipumba alimwandikia barua
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutengua barua yake ya kujiuzulu
na kutaka arejee kwenye kiti chake, uamuzi uliozusha mtafaruku huku Mkutano
Mkuu wa chama hicho ulioketi Agosti 21 ukiridhia kujiuzulu kwake licha ya kuwa
ulivunjika.
“Barua yangu inajieleza sina haja ya
kuichambua. Nimekujibu baada ya kuona mjadala huo (katika mitandao) nilitegemea
(waliomtukana) wawashauri CUF cha kufanya badala ya kuanza kunitukana,” alisema
Jaji Mutungi.
“Sasa huko mahakamani wanakotaka kwenda
kama mahakama ikiamua kama Mutungi alivyoshauri huko nako watatukana pia?” alihoji.
Wanasiasa na wasomi
Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Constatine
Akitanda alisema alichofanya msajili ni kupandikiza zogo ndani ya CUF jambo
ambalo linasikitisha.
Akitanda alisema ndani ya CUF kuna bundi ambaye
alikuwa anasumbua watu ila msajili ameongezea mgogoro huo na kuwa alichokifanya
si sawa kwa mujibu wa mamlaka yake.
“Unajua hii nchi inachezewa sana hivi
mtu anajiuzulu mwenyewe halafu anaamua kurejea mwenyewe bila kufuata taratibu
ni aibu, lakini nadhani kuna mkono wa mtu,’ alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira
alisema anachokiona ndani ya CUF ni uwepo wa biashara haramu ambayo inaweza
kuua chama hicho.
Alisema ni wakati mwafaka kwa wafanyabiashara haramu
hao wakajulikana katika pande zote kwani ni aibu kuvumilia kasoro hizo zitawale
vyama vya siasa.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Tanzania Labour
(TLP), Dominata Rwechungura alisema migogoro ndani ya vyama vya siasa ipo,
hivyo ni jukumu la CUF kutatua ili kurejesha amani na upendo kati yao.
Mwenyekiti wa Chama cha United People Democratic
Party (UPDP), Fahimu Dovutwa alisema kinachotokea ni msiba unaoacha pengo ndani
ya CUF na vyama vya siasa nchini.
Dovutwa alisema pia pengo la mwasisi wa CUF,
marehemu Shaban Mloo linaonekana na kuwataka wazee wa chama hicho kukaa ili
kukinusuru chama.
“Huu ni msiba katika siasa za Tanzania,
naomba CUF watafute wazee wao ili waweze kusuluhisha hali hiyo kwa maslahi ya
chama chao kwani pengo la Mloo linaonekana,” alisema.
Katibu wa Habari na Uenezi wa NCCR Mageuzi, David
Kafulila alisema mgogoro wa CUF unaweza kutolewa uamuzi na mahakama pekee kwa
kuwa msajili hana mamlaka ya kufanya alichokifanya. Kafulila alisema msajili
anapaswa kushauri kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na si kama
alivyoelekeza kwani anaongeza mgogoro zaidi.
Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid alishauri CUF
kutumia vikao kumaliza tofauti zao, huku akibainisha kuwa ndani ya chama hicho
kuna viashiria vya udikteta na usultani.
Mbunge wa Tandahimba CUF, Katani Katani alisema kwa
sasa wamethibitisha jinsi Lipumba anavyotumika kwani pamoja na Jeshi la Polisi
kukataza maandamano, wafuasi wa Lipumba waliandamana bila kuzuiwa.
Alisema haiwezekani chama kikaendeshwa kwa ajenda za
watu wachache ambao wanatumikia matumbo yao na makundi yao na si chama.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) Kitivo cha Sheria, Dk. Onesmo Kyauke alisema msajili anakosea na
kuwataka CUF wakimbilie mahakamani kupata haki.
Credit: Jamboleo
Credit: Jamboleo