Zinazobamba

FREEMAN MBOWE AIPOPOA TWAWEZA,NI KUHUSU TAFITI YAKE,PIA AMSHUKIA LIPUMBA AMESEMA ATAVUNA MALIPO YA USALITI WAKE,SOMA HAPO KUJUA



Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amewataka wanachama wa chama hicho na watanzania kwa ujumla kupuuza taarifa za utafiti za wa taasisi ya Twaweza, anaandika Pendo Omary.


Tamko la Mbowe limekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya Twaweza, kutangaza matokeo ya utafiti wake uliopewa jina la ‘Demokrasia, udikteta na maandamano.’

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mbowe amesema Twaweza ni wapiga zumari wanaochaguliwa wimbo na watawala wa kiimla ili kujaribu kufunika aibu inayolikabili taifa letu kwa sasa.

“Hatua zinazochukuliwa na Rais John Magufuli zimeporomosha uchumi wa nchi yetu kwa kiasi cha kutisha. Mapato ya wananchi yameanguka. Uwekezaji wa ndani na nje ya nchi umepungua. Ajira zimepungua kwa kiasi kikubwa na umasikini umeongezeka,” amesema Mbowe.
Ripoti ya utafiti wa Twaweza iliyokusanywa kutokana na wahojiwa 1,602 kati ya tarehe 23 na 29 Agosti, mwaka huu kwa njia ya simu Tanzania Bara, imesema kwamba watu 6 kati ya 10 wamepinga madai kuwa nchi ya Tanzania inaongozwa kidikteta.
Hata hivyo Mbowe amesisitiza kuwa, kwa sasa mifumo ya kikatiba na kisheria ya uendeshaji wa nchi na serikali imevurugwa kwa kiasi ambacho nchi inaendeshwa kwa amri na vitisho vya mtu mmoja.
Aidha, Mbowe amesema Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya Chadema inatambua mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi- CUF, unaomhusisha aliyekuwa Profesa Ibrahim Lipumba unachochewa na Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Jaji Mutungi anaivuruga CUF kwa kujaribu kumrudisha madarakani Prof. Lipumba, ambaye alijiuzulu madarakani katika mazingira yanayoashiria kununuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa lengo la kusaliti vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Chadema hatumtambui Prof. Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF Taifa au Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, tunamtambua kama adui wa demokrasia na msaliti wa harakati za kudai haki katika nchi yetu,” amesema Mbowe.
Mbowe ameongeza kuwa, Jaji Mutungi pia ni adui wa demokrasia ya vyama vingi na kwamba Chadema haitampa ushirikiano wowote isipokuwa ule tu unaolazimishwa na matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa.
Kuhusu uzinduzi wa oparesheni ya Ukuta iliyotarajiwa kuzinduliwa tarehe 1 Oktoba, mwaka huu, Mbowe amesema mikutano na maandamano hayo yatafanyika kwa siku na tarehe itakayopangwa hapo baadaye kwa kuzngatia hali halisi ya kisasa itakayokuwepo nchini.